Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa

ps@tamisemi.go.tz

Nchi yetu  ilipata uhuru tarehe 09.12.1961 ambapo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alimteua  Mhe.Job Lusinde Waziri wa Kwanza wa Wizara ya Serikali za Mitaa, akifuatiwa na Mawaziri 22  wakiwemo wanawake 3. Kwa sasa Wizara hiyo inaongozwa na Mhe Mohamed Mchengerwa

Tangu mwaka 1961 hadi sasa  Ofisi ya Rais –TAMISEMI imekuwa ni Wizara inayojitegemea, Wizara chini  ya Ofisi ya Waziri Mkuu na kwenye Ofisi ya Rais kama ilivyo sasa. Uamuzi  wa wapi inawekwa umekuwa ukifanyika ili kuimarisha utendaji wa Ofisi  hii.

Ofisi ya Rais TAMISEMI ni Wizara pekee ambayo Makao Makuu  yake yalianzia Jijini Dodoma tangu mwanzoni mwa miaka ya sabini tangu  Serikali ilipotangaza Makao Makuu ya Serikali kuwa ni Dodoma na kwa Dar  es salaam kumekuwa na Ofisi ndogo. Uwepo wa Makao Makuu Dodoma ulikua na  lengo la kutoa fursa sawa kwa wadau wake wakuu hususan Mikoa na Mamlaka  za Serikali za Mitaa kufika Dodoma kwa urahisi wanapofuata huduma  mbalimbali.

Madhumuni ya kuwepo kwa Serikali za Mitaa ni kupeleka  Madaraka kwa Wananchi ambapo chimbuko lake ni Katiba ya Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika Sura ya 8, Ibara ya 145 na  146. Upelekeaji wa madaraka kwa wananchi unapitia katika Mamlaka za  Serikali za Mitaa na ndiyo maana Serikali za Mitaa na ushirikishwaji wa  Wananchi katika mchakato wa maendeleo vimetambuliwa katika Katiba na  Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakati Nchi yetu inapata  uhuru wake kulikuwa na majimbo kumi ya Utawala ambayo yaliritihiwa toka  utawala wa kikoloni wa Kiingereza mwaka 1966. Rais wa kwanza Hayati  Julius Kambarage Nyerere kwa Mamlaka aliyopewa aliunda Mikoa 15 na  kuondoa utaratibu wa mgawanyo wa nchi katika Majimbo. Hadi Sasa Nchi  yetu ina Mikoa 26, Wilaya 139, Halmashauri 184, Tarafa 570, Kata 3,956,  Vijiji 12,319, Vitongoji 64,384 pamoja na Mitaa 4,263. Baada ya uhuru  Halmashauri zilikuwa jumla 45 na hadi kufikia mwaka 2009 zilikuwa  Halmashauri 129 na zimeendelea kuongezeka hadi kufikia 184 mwaka 2021.

Wakati  wa Uhuru hakukuwa na Halmashauri za Majiji na sasa kuna Halmashauri za  Majiji 6, kulikuwa na Halmashauri ya Manispaa moja ya Dares Salaam na  sasa kuna Halmashauri za Manispaa 20, Halmashauri za Miji zilikuwa 9 na  sasa Halmashauri za Miji ni 21 na Halmashauri za Wilaya zilikuwa 10 na  sasa zipo Halmashauri za Wilaya 137.

Serikali iliendelea na  mfumo wa Serikali za Mitaa uliorithiwa kutoka kwa Wakoloni na kuutumia  kama nyenzo za kuleta maendeleo kwa misingi ya Kidemokrasia. Kutokana na  changamoto mbalimbali zilizoukabili utendaji wa Mamlaka za Serikali za  Mitaa baada ya uhuru mwanzoni mwa miaka ya sabini, Serikali ilifuta  Mamlaka hizi na kuanzisha mfumo wa Madaraka Mikoani.

Mfumo huu  ulizifanya Serikali za Mitaa kuitegemea Serikali Kuu kwa kila jambo  kutokana na wananchi kutoshiriki katika maamuzi na pia katika shughuli  za maendeleo, uchumi wa nchi ulididimia na viwango vya maisha kushuka.  Kutokana na hali hii, Serikali za Mitaa kwa upande wa Mamlaka za Miji  zilirejeshwa tena mwaka 1978 na mwaka 1984 Serikali za Mitaa  zilirejeshwa upande wa Mamlaka za Wilaya pia zilirejeshwa.

Kwa  lengo la kuziimarisha Serikali za Mitaa na kuziwezesha kutoa huduma bora  kwa wananchi, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali. Mojawapo ya  hatua hizi ni kuanzishwa kwa Mpango wa Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali  za Mitaa ulioanzishwa mwaka 1998 ambao ulilenga katika kupeleka madaraka  kwa Wananchi (D by D).

Katika kipindi hicho cha Maboresho,  Serikali ilitoa Tamko la Kisera la Ugatuaji wa Madaraka- Policy Paper on  Local Government Reform Programme on Decentralization by Devolution  (D-by-D) kama njia muafaka ya kufikisha na kuharakisha maendeleo ya  Kijamii na Kiuchumi na kuinua utoaji wa huduma kwa wananchi. Uamuzi huu  wa kisera umelenga kuondokana na mapungufu yaliyokuwepo katika Mifumo ya  awali na kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizokuwepo.

Dhana hii  ya D by D imejengwa kwa misingi ya kutoka kwenye mfumo wa Madaraka ya  Serikali Kuu kuwa na maamuzi yote na Serikali za Mitaa kuwa Mtekelezaji  tu (yaani Mwagizaji na Mtekelezaji) kwenda katika mfumo wa Serikali za  Mitaa wenye Mamlaka ya Kisheria ya kuamua mambo katika eneo lao na  kuyatekeleza. Hivyo, kuwa na mfumo wa mahusiano ya majadiliano katika  utekelezaji wa shughuli za maendeleo. Dhana hii inalenga kupeleka  madaraka zaidi kwa wananchi.

Our Latest Jobs

;